Politics

Sunday, November 1, 2015

TUUNGANE PAMOJA

Ndugu zangu watanzani, wapenda mabadiliko, haswa ninyi nyote mliofanywa wanyonge katika nchi yenu kwa dhuluma na manyanyaso mengi tunayoyapata kwa ajili ya kudai haki zetu, niwaombe tu kuwa hatuna sababu ya kuhuzunika wala kusononeka kwa yanayotokea sasa hapa nchini mwetu.

Ifahamike kuwa, haya yanayotokea si bahati mbaya, bali yamekusudiwa kabisa yatokee ili kuturudisha nyuma katika harakati zetu za kudai haki zetu ambazo zimekuwa zikikanyagwakanyagwa ovyoovyo na watawala hapa nchini kwetu Tanzania. Ikumbukwe kuwa hakuna utawala wowote duniani uliowahi kushindana na umma wa watu wake kisha ukashinda. Iwe kwa mabomu au kwa risasi hakuna kabisa!

Kazi yetu ya ukombozi ndo kwanza imeanza rasimi, hivyo hatuna sababu ya kukata tamaa wala kunyong’onyea. Tukifanya hivyo tutakuwa tumetimiza lengo lao, kwani wanafanya hivyo ili kudhoofisha ari yetu ya kuendelea kudai usawa katika jamii yetu.

Najua kuwa kuna nyakati tofautitofauti ambazo tulihitilafiana kimitazamo, hili si jambo baya katika maisha, kwani kwa kuhitilafiana kwetu imetupa nafasi ya kutafakari misimamo ya kila mmoja wetu na kuona mantiki iliyokuwemo katika kila mtizamo, nina imani hiyo imetuimarisha zaidi kuliko ilivyotudhoofisha. Na niseme tu kuwa, kila wakati tulipohitilafiana ulifika wakati tuliafikiana. Sasa niwaombe kwa unyenyekevu mkubwa kabisa kwamba sasa wakati umefika wa kuweka pembeni tofauti zetu na kuunganisha nguvu zetu zote katika suala zima la kudai haki zetu na heshima yetu kama watanzania. Hakuna wakati ambao tunahitajiana zaidi kuliko wakati huu, umoja wetu ni nyenzo muhimu zaidi wakati huu kuliko wakati mwingine wowote katika katika historia ya nchi yetu, tunauhitaji sana ili kufikia malengo yetu, tofauti zetu hazina sehemu kabisa katika kujenga jamii yetu kwa saa, kwani hizo ndizo zimekuwa na zitaendelea kuwa silaha ya kutuangamiza inayotumiwa na utawala huu dhalimu na wenye ghiliba nyingi, hasa kwa watu waliofanywa wajinga kwa makusudi kabisa ili kuudumisha utawala huu ambao mimi siogopi kuuita kwa jina lake halisi bila kuogopa chochote, kuwa ni utawala wa dhuluma na wa kishetani.

Kwanini utawala huu nauita dhalimu na wa kishetani? Kuna mifano chungu nzima inayouweka utawala huu katika kundi la tawala dhalimu duniani.

MANYANYASO DHIDI YA RAIA WAKE.
Kwa miaka kama kumi sasa, tumeshuhudia wananchi wakihangaika huku na kule kwa kuhamishwa katika maeneo yao wanakoishi, huku nyumba zao zikibomolewa bila huruma wala kujali gharama walizozitumia kujenga na mashamba yao kuharibiwa na ardhi yao kuporwa kwa visingizio mbalimbali ikiwemo kupisha uwekezaji ambao hata hivyo haujawahi kuwasaidia wenyewe bali watawala na vibaraka wao ndio wafaidika wakuu wa udhalimu huo. Zaidi ya hayo ifahamike kuwa, watu hawa hujenga baada ya kufuata taratibu zote na mara nyingi huwa an vibali vya kufanya hivyo. Lakini pamoja na hayo hujikuta wakikumbana na adha na misukosuko ya kubomolewa nyumba zao na mashamba yao kuharibiwa. Mfono mwingine; mpaka leo ndugu zetu wenye jamii ya Kimasai waishio Ngorongoro wanatakiwa waondoke au wakose haki yao ya kufanya shughuli za uzalishaji kisa uwekezaji ambao haujawapa faida wakazi wa Ngorongoro kwani bado wapo kwenye umasikini mkubwa.

Pia, tumeshuhudia wananchi ambao ni wafanya biashara wakilazimishwa kununua mashine za kutoza kodi kutoka kwa mzabuni, licha ya kuwa dunia ya sasa ni huru ambayo inaruhusu mtu anunue kitu mahali anapokitaka kwa bei anayoitaka. Hawa walilazimishwa kununua mashine hizi kwa bei ambayo ni mara mbili ya bei halisi, na walipohoji waliishia kupigwa mabomu, kufunguliwa mashitaka na kusababishiwa tafrani kubwa.

Tumeshuhudia wanafunzi wa vyuo vikuu wakiishia kuvunjwa miguu na kupigwa mabomu ya machozi karibu kila wakati, kwa kudai posho ya chakula ambayo serikali iliwaahidi kuwalipa na wala isifanye hivyo, licha ya ukweli kuwa vijana hawa wanatoka mikoani na hawana namna mbadala ya kupata pesa za kuishi zaidi ya hizo ambazo ziliahidiwa na serikali, hili lilipelekea mpaka vijana wengi wafukuzwe vuoni na baadhi ya vijana wa kike wajiingize kwenye biashara za kuuza miili yao ili wajikimu, ingawa nyoyo zao hazikuwa radhi kufanya hivyo.

Tumeshuhusia polisi wakiua watu wasio na hatia, wakiwepo waandishi wa habari, kwa matakwa ya watawala na kwa kuthibitisha hilo, hatujawahi ona hata polisi mmoja akitiwa nguvuni kwa kosa la mauaji, hii inadhibitisha kuwa wapo wenye maguvu waliowatuma!

Tumeshuhudia wananchi wakiporwa haki yao ya kuchagua kiongozi wanayemtaka, badala yake hulazimishwa kuongozwa na kiongozi wasiyemchagua. Na kama walifanikiwa kumpata kiongozi waliyemchagua kwa hiari yao, basi ilikuwa ni lazima wahatarishe maisha yao, kwa kukesha kwenye vituo vya kuhesabia kura, kupaza sauti zao kuhimiza matokeo yatangazwe huku wakikabiliana na viumbwa vya watawala na hata wakati mwingine iliwabidi wafanye fujo, hapo ndo walifanikiwa kupata kiongozi waliyemtaka, zaidi ya hapo waliishia kupewa kitu tofauti kabisa na walichokichagua.

Tumeshuhudia wananchi wa Mtwara wakikabiliana na kipigo kikali kutoka jeshi la wananchi wa Tanzania (ambalo mimi nachelea kuliita hivyo badala yake naona afadhali lingeitwa jeshi la watawala), kwa kisingizio cha kuto tii sharia bila shuruti. Kisa walihoji uporwaji wa rasilimali gesi yao ambayo Mungu aliiweka kule kwa makusudi ya wao kunufaika nayo. Wao kwa maoni yao walitaka isafishiwe palepale ili wapate ajira na wala si kuzuia isiwafikie wananchi wengine.

Tumeshuhudia watu wakipigwa risasi za moto eti walikaribia eneo la mwekezaji kule Nyamongo na maeneo mengine mengi yanapochimwa madini.

Tumeshuhudia wananchi wakikosa haki yao ya uwakilishwaji kwenye vyombo vya maamuzi kwani viongozi waliolazimishiwa, hawakuwajibika kwao bali waliwajibika kwa watawala waliolazimishia kupatikana kwao, kwa masilahi yao wenyewe, hivyo wananchi kukosa wa kumtuma au kumwajibisha kwa lolote lile, jambo lililopelekea uzorotaji wa maendeleo katika maeneo mengi nchini, huku viongozi vibaraka wa watawala wakijichukulia mishahara, posho na marupurupu kibao wasiyoyatolea jasho kwa kodi za wananchi wavuja jasho! Huu ni unyanyasaji mkubwa.

Tumeshuhudia ufisadi wa pesa za umma wa kiwango cha kupindukia, ambao hata baada ya ushahidi kuonyesha wahusika ambao pesa hizo zilitiwa kwenye akaunti zao hawakuchukuliwa hatua yoyote na watawala, hii ina maana kuwa watawala walikuwa sehemu ya wizi huo.

Linaloshangaza ni kuwa, waakati wananchi wakifanyiwa haya yote hawakutakiwa waseme chochote, yaani iliwabidi wanyamaze kimya wakati wakifanyiwa dhuluma na unyanyasaji huu. Walipojaribu kuamka na kuzilalamikia mamlaka husika walikutana na mabomu ya machozi na risasi za moto na wengine kuishia vizuizini. Ama kweli watanzania tumenyanyasika vya kutosha.

KUKOSEKANA KWA HUDUMA MUHIMU
Tumeshuhudia wananchi wakikosa huduma muhimu na za msingi, kama vile afya, umeme maji na elimu bora licha ya kutozwa kodi kubwa katika manunuzi yao, na katika biashara zao. Hospitali hazina dawa, shule hazina waalimu maabara wala vitabu vya kutosha havipo.

Vifo vya akina mama na watoto vinaendelea kuwa tishio. Wananchi wa kawaida ndo wanaotozwa kodi kubwa zaidi kuliko wafanya biashara wakubwa wanaosamehewa kodi. Lakini pamoja na kuwatoza kodi kubwa kiasi hicho hawapati huduma zinazolingana na kodi zao, kinyume chake pesa zinaingia katika mikono ya mafisadi na mwananchi hatakiwi kuhoji.

Watoto wakitanzania wengi wanakabiliwa na tatizo la udumavu. Ambao uko kwa kiwango cha asilimia 45% ya watoto wote! Udumavu ni matokeo ya kutokula chakula bora na kilichokamilika! Baada ya miaka 50+ ya Tanzania kujitawala bado tuna tatizo la njaa kwa kiwango cha kuwepo na watoto wenye udumavu kwa asilimia 45%! Hii ni kwa mujibu wa tafiti za hapa karibuni zilizofanya na twaweza. Nafikia mahali najiuliza kuwa je jambo hili ni bahati mbaya au lafanywa kwa makusudi? Udumavu, licha yakuathiri ukuaji wa mtoto kwa umbo na kimo, pia huathiri uwezo wa kufikiri wa mtoto husika na hali hii huendelea hata katika utu uzima wake. Ndiyo maana tuna watu wengi kwenye jamii wasio na uwezo wa kuhoji wala kutafakari mambo kwa kina. Hili laweza kuwa ni moja kati ya matokeo ya udumavu wa utotoni wa watu hawa. Hapa tena najiuliza kuwa, labda kuwepo kwa tatizo hili ni sehemu ya mkakati wa kutufanya tuwe na uwezo mdogo wa kufikiri ili watawala waendelee kututawala? Ebu tulitafakari hili kwa mapana na marefu yake.

Tofauti ya huduma za elimu baina ya watoto wa watawala na makabwela nayo ni ya kutisha na inatia shaka kama kweli na wengine wamekusudiwa wawe na elimu yenye kuleta ushindani katika soko la ajira. Kwa mtazamo wangu naona hili nalo limetengenezwa ili kuwafanya hawa watoto wa kabwela wajione nao wanapata elimu lakini kiuhalisia siyo hivyo, kwamba hawapati elimu halisi.

HAKUNA HAKI KATIKA VYOMBO YA UTOAJI HAKI
Tumeshuhudia mtu mnyonge akiishia kufilisika zaidi, kama ataamua kwenda kudai haki katika vyombo vya haki naau atika ofisi za umma. Kwanza, atazungushwa weee, pili atadaiwa rushwa, mwisho ataambiwa haki ile si yake licha ya kuwa amepoteza muda mwingi na pesa nyingi. Masikini wanasingiziwa kesi ili wakishindwa kesi hizo waporwe vitu vyao ikiwemo ardhi. Haki imekuwa ni kwa ajili ya matajiri wakubwa na watawala tu.

UPORAJI WA DHAHIRI WA RASILIMALI ZA TAIFA
Tumeshuhudia idadi ya ndovu wetu ikipungua kwa kazi ya ajabu. Tumeshuhudia Twiga wakipakiwa kwenye madege wakiwa hai, tumeshuhudia shehena za meno ya tembo zikikamatwa, lakini hatujawahi kujua wahusika wamepelekwa wapi na wamepewa adhabu gani kwa kosa hilo. Tumesikia katika kona zingine za nchi magogo yakisafirisha nje ya nchi wakati watoto wetu kwa idadi kubwa kabisa bado wanakaa chini kwenye shule zao. Watu wengi bado wanaishi katiak nyumba za nyasi au makuti. Tumesikia nchi zingine zikipata tuzo za kidunia za uuzwaji wa madini ambayo hayako sehemu nyingine duniani isipokuwa hapa kwetu!

JE KUNA NIA YA DHATI YA KULETA USAWA KWENYE JAMII?
Kwa kifupi ni kuwa, hakuna nia! Siyo tu kwamba hakuna nia ya dhati ya kuleta usawa katika jamii, bali hata hiyo nia isiyo ya dhati haipo. Hawa mabwenyenye wamekusudia kututawala kiunyonyaji na hawana hata chembe ya huruma na wala hawana kusudio la kuleta usawa katika jamii yetu ya kitanzania, bali wameendelea na mradi wao wa kutuweka katika matabaka ya watawala na watawaliwa, walionacho na wasionacho, vibaraka wa watawala na wasio vibaraka wa watawala! Hili linadhihirika wazi pale watawala wanapotumia nguvu kubwa sana ya kuzuia matakwa ya umma wa watanzania ya kujikomboa. Wanatumia kila aina ya mbinu, nguvu na hila.

Kwa muda mrefu sasa, baada ya wananchi kuchoshwa na mateso yanayofanywa na utawala huu uliokubuhu kwa dhuluma, wananchi wamekuwa wakipaza sauti zao kupigania kuwepo kwa katiba mpya, ambayo ingeziba mianya ya rushwa na ufisadi, ambayo ingetoa fursa kwa mnyonge naye kunufaika na rasilimali zake, ambayo ingempa mwananchi mamlaka ya kumwajibisha kiongozi wake, ambayo ingeweka maadili na miiko ya uongozi, ambayo ingekuza uwajibikaji, ambayo ingempa mwananchi haki ya kuchagua kiongozi amtakaye, ambayo ingeboresha maisha ya mtu mdogo, ambayo ingeondoa hali ya umungu mtu miongoni mwa watanzania na kuwaweka watu katika hali ya usawa na  amboyo ingewezesha kuwepo kwa vyombo huru vya kiutendaji na vya kimaamuzi.

Kwa kuona hitaji hilo, wananchi walianzisha mchakato wa kuiandika katiba hiyo mpya. Na baada ya kelele nyingi za wananchi watawala wakaona wafanye geresha na kuruhusu mchakato uanze, hali wakijua kabisa kuwa hawataki hilo litokee! Wakaruhusu sharia zitungwe, vyombo viundwe na wananchi waulizwe maoni yao juu ya katiba waitakayo. Vyote hivyo vilifanyika na wananchi wakatoa maoni yao ambayo yalikuja kuwekwa kwenye rasimu ya pili ya katiba chini ya mzee Warioba na watu wakaona huo ungekuwa mwanzo mpya wa taifa lao kujijenga upya na kuwa na usawa katika jamii! Lakini kama mlivyoona, kwa macho makavu kabisa yaso na chembe ya haya hawa mabwenyenye waliitupilia mbali katiba ile na wala hawakujali maoni ya wananchi, waliyapuuza vikali licha ya kuwa pesa nyingi za walipa kodi zilikuwa zimeshaliwa. Waliishia kufanya maigizo, kwa matisho mkubwa, ya kitu kilichoitwa katiba pendekezwa ambacho nacho hakikufika popote na ndiyo ilivyokusudiwa iwe!

Kwa sababu hiyo sasa, kuna haja ya sisi wananchi kuendelea kudai katiba mpya bila kusubiri hisani ya hawa wadhalimu. Hii iwe kampeni endelevu na hapa tusiwaachie watawala watupangie namna ya kudai hili, kwani watatuchelewesha kwa makusudi maana wao hawaitaki katiba mpya, katiba mpya kwao ni msalaba mzito, hawataihimili kwa kiwango cha maovu yao. Ni lazima iwe ni sisi wananchi tutakaoidai na si vinginevyo, watawala hawaitaki, inawakatia mirija ya kutunyonya, tusitarajie kuwa watakuwa na kiwango hicho cha wema, kwanza wema si hulka yao! Sisi wenyewe ndio tutakao fanya shinikizo la kuwepo kwa katiba mpya na bora kwa masilahi ya umma mkubwa wa watanzania! Tuanze sasa na mimi kwa kuonyesha mchango wangu katika hili nimeanzisha kampeni inayoitwa, KATIBA MPYA SI ZAWADI, NI HAKI YETU TUIPEWE! Nitaendelea kupigania hili na niwaombe kila mmoja wetu, kwenye vikundi mbalimbali, kwenye mitandao tuendeleze harakati hizi za kudai katiba na pia niwaombe mniunge mkono kwenye kampeni hii niliyoianzisha.

MUNGU IBARIKI TANZANIA, MUNGU IBARIKI AFRICA.

No comments:

Post a Comment